KAULIMBIU:  Kiswahili - Mhimili wa Umoja, Maendeleo ya Elimu na Uchumi.

Maswali Yanayoulizwa mara kwa mara


Hapana, BAKITA tunao wafasiri wa lugha za Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kireno na Kiarabu. Kwa lugha nyingine tunatumia wafasiri wa nje ambao sio waajiriwa wa Baraza. Wafasiri hao wameidhinishwa na wanafanya tafsiri kwa niaba ya Baraza.
Baraza lina idara ya uchapishaji ambayo moja ya majukumu yake ni kuwasaidia waandishi chupukizi ili kuwajengea stadi nzuri za uandishi na kuwapa maelekezo ya namna ya kuandika kazi nzuri na zenye mvuto kwa jamii.
Baraza hutumia vyombo vya habari kuelimisha umma kuhusu usahihi wa lugha. Aidha, Baraza huandaa vitabu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kamusi, jarida la lugha yetu, Jifunze Kiswahili Uwafunze wengine ili kuwasaidia umma kutumia lugha kwa usahihi.
Baraza limekusanya kanzi data ya wataalamu wa lugha ya Kiswahili katika uga wa ualimu, tafsiri na ukalimani. Pale kutakapokuwa na mahitaji, Baraza litatumia kanzi data hiyo kuwapata wahusika. Hata hivyo, Baraza linawahimiza Watanzania kuwa wepesi na wadadisi wa mambo ili kubaini haraka mahali panapohitajika wataalamu wa Kiswahili hususani kwa kutumia mitandao kutafuta nafasi hizo.
Baraza limeandaa Kanuni za Sheria yake ambazo zitalipa mamlaka kisheria ya kuwatoza faini au kuwachukulia hatua zinazostahili wale wote wanaoharibu lugha. Hatua hizo zitachukuliwa baada ya Baraza kupitia hatua kadhaa za kuwaandikia au kuonana na wahusika ana kwa ana na kuwaeleza kuhusu jambo hilo. Ikiwa hilo litaendelea hata baada ya kupewa onyo mara tatu sheria itachukua mkondo wake.
Baraza huandaa semina maalumu kwa ajili ya waandishi wa habari na pia huandaa makongamano kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu utumiaji sahihi wa lugha. Aidha, Baraza limeandaa vitabu mbalimbali kikiwemo kitabu cha Mwongozo kwa Waandishi wa Kiswahili Sanifu ambacho maudhui yake yanalenga kuwasaidia waandishi kuandika kwa usahihi na kwa kuzingatia kanuni za uandishi.
Baraza hutoa huduma kwa watu walio mbali kwa njia ya simu, barua za kawaida na barua pepe.
BAKITA kirefu chake ni Baraza la Kiswahili la Taifa. Baraza liliundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 27 ya mwaka 1967 na kufanyiwa marekebisho mwaka 1983.
Baraza hutumia vyombo vya habari pamoja na shughuli mbalimbali zinazohusisha wataalamu na wanajamii kwa ujumla kutangaza shughuli zake. Shughuli ambazo Baraza hutumia kutangaza kazi zake ni kama vile makongamano, warsha n.k. Baraza pia huandaa vipeperushi vinavyoeleza shughuli za Baraza na kuvisambaza kwa wanajamii.
Baraza lina kamusi moja ya Kiswahili- Kiswahili ambayo ni Kamusi kuu ya Kiswahili, kamusi ya Istilahi za Kiswahili na kamusi nyingine ndogondogo za taaluma mbalimbali.
Baraza huzuia upotoshaji wa lugha kwa kuelimisha jamii kuhusu utumiaji sahihi wa maneno. Hutoa elimu hiyo kupitia vyombo vya habari na wakati mwingine kuandikia barua taasisi, shirika au kampuni zinazoharibu lugha kwa kuonyesha maneno yanayobanangwa pamoja na masahihisho yake.
Baraza hufuatilia matumizi ya maneno linayoyaunda katika jamii kwa kusikiliza watumiaji lugha kwa ujumla pamoja na kusikiliza vyombo vya habari kuona iwapo maneno hayo yanatumika sawasawa.
Istilahi zinazoundwa na Baraza husambazwa kwa watumiaji kwa njia zifuatazo:
i. Vyombo vya habari: Baraza hutumia vyombo mbalimbali kama vile magazeti, redio na televisheni kusambaza maneno linayoyaunda. Kwa mfano Vipindi vya redio na Televisheni - Baraza huendesha vipindi mbalimbali vya Kiswahili katika televisheni na redio mbalimbali m.f. TBC Taifa, Redio One, Clouds, Redio Mlimani n.k. na televisheni kama vile TBC 1 ambapo hutumia fursa hiyo kunadi maneno mapya yaliyoundwa na pia kufuatilia matumizi yake. Baraza pia hutoa Makala mbalimbali katika gazeti la Habari leo, Makala hizo huelezea namna sahihi na miktadha ya utumiaji wa maneno mbalimbali ya Kiswahili.
ii. Mikusanyiko ya wadau mbalimbali wa Kiswahili: Baraza hutumia shughuli zinazowakutanisha wadau mbalimbali wa Kiswahili m.f. makongamano na warsha kunadi maneno mapya na pia kupata mwitiko wa matumizi ya maneno hayo kutoka kwa wadau hao.
iii. Vitabu: Baraza huandaa matoleo mbalimbali ya vitabu vyenye istilahi zake na hivyo wanajamii huweza kujifunza maneno hayo kupitia vitabu hivyo.
Baraza linatumia mbinu mbalimbali katika kuunda na kusanifisha maneno mapya ya Kiswahili, miongoni mwake ni kama vile: Utohozi m.f. kompyuta, Tafsiri m.f. free market- soko huria, Ufupishaji au akronimu m.f UKIMWI – Ukosefu wa Kinga Mwilini, Uhulutishaji; njia ambayo inahusiana sana na akronimu m.f. Chajio – Chakula cha jioni, Uambishaji m.f, a- na-som-a, som-w-a a-na-m-som-e-a, u-na-ye-m-som-e-a, Unyambulishaji m.f. som-a, som-e-a, som-w-a, som-ek-a, som-e-an-a. Uambatishaji m.f. mwanaanga, na Urudufishaji m.f. polepole. Aidha, katika uundaji wa maneno mapya mbinu nyingine inayotumika ni kurudi kwenye hazina ya Kiswahili chenyewe. Mbinu hii ni ile ya kuchota maneno kutoka kwenye lahaja za Kiswahili m.f. Kipemba, Kitumbatu, Kimrima, Kimvita n.k. Maneno pia hutafutwa katika lugha nyingine za kibantu, Kiafrika na ikitokea yamekosekana hutafutwa kwenye lugha nyingine za nje.
Machapisho ya BAKITA hupatikana katika sehemu zifuatazo:
i. Ofisi za BAKITA.
ii. Maonyesho, kama vile ya Sabasaba, Nanenane, Wiki ya Utumishi wa Umma n.k.
iii. Mikutano na Makongamano yanayohusu Lugha ya Kiswahili na Utamaduni wa Mtanzania.
BAKITA linachapisha machapisho ya aina mbalimbali kama vile:
i. Kamusi za aina mbalimbali.
ii. Vitabu vya Sarufi, Fasihi
iii. Historia ya Kiswahili.
iv. Vitabu vinavyohusiana na Matumizi ya kila siku ya lugha.
v. Tafsiri Sanifu.
vi. Vijitabu vya lugha tatu.
vii. Vitabu vya miongozo kwa waandishi.
viii. Vitabu vya Kiswahili kwa Wageni.
BAKITA halichapishi vitabu vya waandishi mbalimbali badala yake huchapisha vitabu vyake lenyewe.
Mchapishaji hushughulika na mchakato mzima wa kuandaa na kufuata taratibu za mswada kuwa kitabu pia kulinda haki za mwandishi. Mchapaji anapokea kazi iliyotayarishwa na mchapishaji na kuichapa kuwa kitabu.
Namba ya Kimataifa ya Kitabu (ISBN) hutolewa na Maktaba Kuu ya Taifa kwa kampuni/mashirika ya uchapishaji, mwandishi ataipata namba hiyo kwa mchapishaji atakayeingia naye mkataba wa kuchapisha kitabu chake.
Mwandishi chipukizi apitie hatua zifuatazo:
i. Awe na uelewa wa kile anachotaka kukiandika (riwaya, tamthiliya, hadithi fupi, ushairi n.k.).
ii. Aandike rasimu ya kwanza.
iii. Awasiliane na BAKITA hii kwa ajili ya kuhaririwa na kupewa ushauri kuhusu kazi yake.
iv. Afanye marekebisho ya kazi yake kulingana na ushauri aliopewa na BAKITA.
v. Awasiliane na mchapishaji kwa ajili ya makubaliano ya kimkataba.
vi. Achapishe kazi yake.
Mambo yanayoangaliwa ni:
i. Aina ya mswada.
ii. Muundo wa mswada.
iii. Maudhui ya mswada.
iv. Ufasaha wa lugha iliyotumika.
v. Usahihi wa alama za uandishi na matumizi ya herufi kubwa na ndogo.
vi. Wahusika waliotumika katika mswada.
vii. Walengwa wa mswada.
viii. Kufaa au kutofaa kwa mswada.
Ndiyo, tunaratibu na kutoa huduma za Ukalimani na Tafsiri kwenye mikutano ya kitaifa na kimataifa na katika shughuli za makampuni, mashirika na watu binafsi. Mteja anapokuwa anahitaji wakalimani kwa ajili ya mkutano anawasiliana nasi na tunampa majina ya wakalimani ambao atawasiliana nao na watamueleza taratibu na gharama za kufanya ukalimani.
Mteja haruhusiwi kutafsiri kazi yake yeye mwenyewe hata kama lugha anaifahamu, pia haruhusiwi kupeleka kwa mfasiri yeyote ambaye hajaidhinishwa na Baraza. Baraza linathibitisha na kugonga muhuri tafsiri ambazo zinatoka kwa wafasiri waliyoidhinishwa na Baraza tu.
Tunatoa huduma ya kutafsiri vyeti vya kuzaliwa, shule, ndoa, kifo n.k kwa lugha mbalimbali. Pia tunatoa huduma ya kutafsiri miswada mbalimbali, vitabu, mikataba n.k kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili na Kiswahili kwenda Kiingereza. Pia tunapitia na kuthibitisha tafsiri zilizofanywa na wafasiri wa nje. Baraza pia linatoa huduma ya kupitia kazi ambazo zimeshatafsiriwa nje kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili kwa gharama ya Tsh 10,000 kwa ukurasa. Ili kupokea kazi hizo inabidi kwanza tuhakikishe aliyetafsiri ni mtaalamu na tunachofanya ni kurekebisha makosa madogo ya kisarufi na msamiati. Hatupokei kazi ambayo imetafsiriwa vibaya kiasi cha kutulazimu kuirudia upya.
Hapana, BAKITA tunao wafasiri wa lugha za Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kireno na Kiarabu. Kwa lugha nyingine tunatumia wafasiri wa nje ambao sio waajiriwa wa Baraza. Wafasiri hao wameidhinishwa na wanafanya tafsiri kwa niaba ya Baraza.