KAULIMBIU:  Kiswahili - Mhimili wa Umoja, Maendeleo ya Elimu na Uchumi.BARAZA LA KISWAHILI LA TAIFA (BAKITA) KUWA NA KANZIDATA YA WATAALAMU WA KISWAHILI


Imechapishwa Jumanne, 29 Agosti 2017Baraza la Kiswahili la Taifa lilifanya mkutano na waandishi wa habari tarehe 28/08/2017 kufafanua tangazo lake lilitolewa katika mitandao ya kijamii. Tangazo lake lilihusu uanzishaji wa kanzidata ya wataalamu wa Kiswahili.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Dkt. Selemani S. Sewangi aliwaeleza waandishi wa habari azima ya Baraza ya kuwa na kanzidata ya wataalamu wa Kiswahili. Alieleza kwamba, kuwa na wataalamu wa Kiswahili ni jambo moja na kuwa na taarifa zao ambazo zinaweza kupatikana haraka pindi zitakapohitajika ni jambo jingine. Pamoja na kwamba Tanzania ina wasomi na wataalamu wengi wa Kiswahili, leo hii sio rahisi kujua wataalamu hao ni kinanani, wana ujuzi wa aina gani na wa kiwango gani, wako wapi na wanafanya nini. Katika hali kama hiyo, sio rahisi kuwapata wataalamu hao pale uhitaji wa haraka unapojitokeza.
Alieleza kwamba ili kukabiliana na tatizo hilo, BAKITA limeamua kukukusanya taarifa za kitaaluma na za kibinafsi za wataalamu wa Kiswahili na kuzihifadhi katika mfumo wa kikompyuta ambao utawezesha kupatikana kwa wataalamu hao pale watakapokuwa wakihitajika.
Taarifa zinazokusanywa ni vivuli vya vyeti vya matokeo ya kuhitimu katika vyuo vikuu na katika taasisi nyingine za mafunzo ya utaalamu husianifu kama vile utaalamu wa ukalimani, tafsiri, ualimu wa Kiswahili kwa wageni na ukalimani wa lugha ya alama kwa Kiswahili. Aidha, wasifu (CV) wa wataalamu hao wenye taarifa mbalimbali kama vile, namba zao za simu, anuani za barua pepe, hali yao ya ajira, lugha nyingine za kimataifa wanazozijua, uzoefu wao katika ajira mbalimbali zinazohusiana na Kiswahili utatakiwa.
Kwa sababu lengo ni kukusanya taarifa za kitaaluma na za kiutaalamu, katika zoezi hili vivuli vya vyeti vya matokeo ya Sekondari, vyeti vya uanachama wa vyama vya Kiswahili, vyeti vya kuhudhuria makongamano na hata vyeti vya kuhitimu havitahitajika.
Taarifa hizo zitairahisishia Serikali kuwapata wataalamu wetu wa Kiswahili na utaalamu husianifu pale itakapowahitaji, ama katika ajira au kwa majukumu mengine ya kitaifa. Vilevile utalirahisishia BAKITA katika uraribu wa mambo mbalimbali yanayohusu wataalamu hao ikiwa ni pamoja na kufanikisha mipango ya mafunzo ya muda mfupi ya msasa katika utaalamu mbalimbali.
Aidha, Dkt. Selemani Sewangi alifafanua kwamba mahitaji ya wataalamu wa Kiswahili kwa hivi sasa yameongezeka sana na hivyo ni muda mwafaka kuwa na kanzidata ya wataalamu hawa ili kuhakikisha kwamba mara tu wanapohitajika wanapatikana. Pia, alitoa mfano wa viongozi mbalimbali waliotembelea nchi yetu mfano Waziri Mkuu wa Ethiopia Heilemariam Dessalegn na Rasi wa Misri Abdel Fattah Elsisi ya kwamba wote walionyesha nia ya kupatiwa walimu wa kwenda kufundisha Kiswahili katika nchi zao.
Alisema kuwa taarifa zilizoainishwa hapo juu zinatakiwa kutumwa kwenye barua pepe ya BAKITA ambayo ni bakita@habari.go.tz na aliwahakikishia wataalamu hao kwamba taarifa zao zitapokelewa na kushughulikiwa inavyopaswa.
Kaimu Ofisa Mawasiliano na Umma,
BAKITA