KAULIMBIU:  Kiswahili - Mhimili wa Umoja, Maendeleo ya Elimu na Uchumi.TANZIA


Imechapishwa Jumatatu, 06 Mei 2019Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya msiba wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni za IPP, Dkt Reginald Abraham Mengi. Dkt. Mengi alikuwa mdau mkubwa wa lugha ya Kiswahili. Pamoja na weledi mkubwa aliokuwa nao katika lugha nyingine alitambua kuwa ni Mtanzania anayepaswa kujivunia lugha yake ya Taifa ya Kiswahili. Marehemu alitumia lugha adhimu ya Kiswahili katika mikutano yake mingi ya fursa na huku akijieleza kwa usanifu na ufasaha kwa kutumia lugha hii. Marehemu ni miongoni mwa waasisi wa vituo vya utangazaji vinavyomilikiwa na watu binafsi ambavyo tangu kuanzishwa kwake vimekuwa vikitangaza kwa Kiswahili na kutoa wasaa maalumu wa kuelimisha umma kuhusu matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili.

Aidha, marehemu alisisitiza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika lebo za bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali hapa nchini. BAKITA limempoteza mwanataaluma muhimu katika mapambano ya kuiendeleza lugha yetu.

Kwa kuwa kuishi ni faida na kifo ni lazima inatubidi tukubali mapenzi ya Mwenyezi Mungu ya kumtwaa mpendwa wetu. Tunatoa pole kwa familia, wafanyakazi wenzake, marafiki na watu wote kwa msiba huu mkubwa.


Bwana alitoa na Bwana ametwaa, Jina la Bwana lihimidiwe.
Wasaalamu
DKT. SELEMANI S. SEWANGI
KATIBU MTENDAJI
BAKITA