KAULIMBIU:  Kiswahili - Mhimili wa Umoja, Maendeleo ya Elimu na Uchumi.ZIARA YA MHESHIMIWA WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO KATIKA OFISI ZA BAKITA


Imechapishwa Jumatano, 16 Agosti 2017Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison G. Mwakyembe (MB) alitembelea ofisi za Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) zilizoko Kitonyama tarehe 15/8/2017 kwa lengo la kuona utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo. BAKITA ni moja taasisi zilizo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Miongoni mwa mambo yaliyojiri ni pamoja na Katibu Mtendaji wa BAKITA Dkt. Selemani S. Sewangi kumweleza Waziri muundo wa Baraza pamoja na majukumu yake. Dkt. Sewangi alifafanua kwamba Baraza lina Idara sita ambazo ni Idara ya Tafsiri na Ukalimani, Uhariri na Uchapishaji, Lugha na Fasihi, Istilahi na Kamusi, Mawasiliano na Umma na Fedha na Uendeshaji. Aidha, alieleza kuwa Baraza pia lina vitengo viwili ambavyo ni Kitengo cha Ugavi na Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani.
Aliendelea kueleza kuwa Baraza limepokea muundo mpya wa BAKITA kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambao unaelekeza Baraza kuwa na Idara mbili ambazo ni Idara ya Mendeleo na Matumizi ya Kiswahili na Idara ya Huduma za Baraza. Idara hizi zitasimamiwa na Wakurugenzi.
Idara ya Mendeleo na Matumizi ya Kiswahili itakuwa na sehemu tatu ambazo ni: Istilahi na Kamusi, Tafsiri na Ukalimani na Idara ya Lugha, Fasihi na Uhariri. Sehemu hizi zitasimamiwa na Mameneja wa sehemu.
Aidha, Katibu Mtendaji aliendelea kueleza kwa kubainisha majukumu ya BAKITA ikiwa ni pamoja na;

 1. Kukuza lugha na fasihi ya Kiswahili

 2. Kukuza msamiati na istilahi za Kiswahili

 3. Kufanya utafiti mbalimbali wa Kiswahili.

 4. Kuhimiza matumizi fasaha ya Kiswahili Sanifu

 5. Kutoa huduma za Tafsiri na Ukalimani kwa Serikali, Makampuni, Mashirika na kwa watu binafsi.

 6. Kutoa mafunzo ya Kiswahili kwa wageni na kwa wahitaji maalumu;

 7. Kutoa huduma za uhariri na ithibati kwa waandishi wa Kiswahili;

 8. Kuchapisha vijarida na majarida kwa ajili ya kusambaza Kiswahili;

 9. Kuanzisha mashindano ya waandishi wa Kiswahili;

 10. Kuendesha semina, warsha, makongamano ma matamasha ya kuenzi Kiswahili na waandsihi wake waliotukuka.

 11. Pia, Katibu Mtendaji alibainisha changamoto mbalimbali zikiwemo majengo ya Baraza kuendelea kukaliwa na waliokuwa wafanyakazi wa Shirika la Bima la Taifa. Alieleza kwamba, mwaka 2009, BAKITA lilinua nyumba za Shirika la Bima la Taifa kwa gharama ya sh. Bilioni moja na nusu (1,500,000,000/-). Hata hivyo, kutoka kipindi hicha Baraza halijaweza kutumia majengo yote lililonunua kwa sababu waliokuwa wafanyakazi wa Shirika hilo (baadhi yao) walifungua kesi katika mahakama kuu kitengo cha Ardhi wakidai wauziwe majengo ambayo tayari yalikwishauziwa BAKITA. Pamoja na kesi hiyo, kutupwa na jaji aliyekuwa akisimamia keshi hiyo, bado kumekuwa na mfululuzo wa kufunguliwa kwa kesi nyingine zenye madai hayohayo na katika mahakama hiyohiyo hadi hivi sasa. Kila mara kesi inapotolewa hukumu na walalamikaji kushindwa, huwa wanafungua kesi nyingine kwa madai hayohayo.
  Changamoto nyingine iliyobainishwa ni Baraza kuwa na watumishi wachache kinyume na ikama halisi inayotakiwa. Baraza kwa sasa lina wafanyakazi 29 wakati ikama yake lilitakiwa kuwa wafanyakazi 83.
  Mheshimiwa Waziri akiongea na wafanyakazi wa BAKITA alieleza kwamba BAKITA ya sasa inapaswa kubadilika na kuwa tofauti na ile ya miaka 1967 wakati lilipoundwa. BAKITA ya sasa iko katika wakati ambapo kuna mahitaji makubwa ya lugha ya Kiswahili. Waziri alieleza kwamba Serikali kwa dhati imeamua kutumia Kiswahili katika shughuli zake zote na hata katika mikutano yake ya ndani na nje pale anapokuwepo mkalimani. Pia alitoa mfano wa nafasi na mahitaji ya lugha ya Kiswahili Afrika na duniani kwa sasa. Alibainisha kwamba tayari Kiswahili kimekubaliwa kutumiwa katika mikutano ya Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki n.k. Aidha, alieleza kwamba kuna mahitaji makubwa ya Kiswahili kutoka katika nchi mbalimbali duniani, hivyo Baraza halina budi kujipanga vema kuhakikisha kwamba mahitaji haya ya lugha ya Kiswahili yanakidhiwa vema.
  Aliagiza Baraza kuandaa kanzi data ya wahitimu wote wa Kiswahili ili data hiyo iweze kutumiwa pale wanapohitajika walimu katika sehemu mbalimbali duniani. Pia, Mheshimiwa Waziri aliagiza kwamba kuwe na jitihada za dhati za kuhakikisha kwamba Baraza linapata fedha za kujiendesha. Waziri alieleza kwamba miongoni mwa taasisi ambazo zinapaswa kuwa na fedha nyingi ni pamoja na BAKITA kulingana na nafasi ya Kiswahili hivi sasa. Alibainisha kwamba yako mambo mengi yanayohusiana na lugha hii ambayo BAKITA linaweza kufanya na kujiingizia kipato. Aliunga mkono jitihada za uandishi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili ambayo italiingiza Baraza mapato lakini alisisitiza kuwa bado ziko nafasi nyingi zinazoweza kutumiwa na BAKITA kupata fedha zaidi ikiwa ni pamoja na kufundisha wageni Kiswahili.
  Mheshimiwa Waziri alisikitishwa sana na kitendo cha waliokuwa wafanyakazi wa Bima kuendelea kukalia nyumba zilizonunuliwa na Serikali kwa lengo la kutumiwa na taasisi hii kama ofisi. Mheshimiwa alisema, nyumba hizo zilinunuliwa kwa kodi za Watanzania na ikiwa Bima waliuza inakuaje nyumba hizo ziendelee kukaliwa? Alihoji. “Kama Bima wanataka nyumba hizi ziendelee kukaliwa na waliokuwa watumishi wake wanapaswa kurejesha fedha zilizonunulia nyumba hizo ambazo ni kiasi cha sh. Bilioni moja na nusu pamoja na riba ya miaka saba tangu majengo haya yaliponunuliwa na malipo yote kukamilika.
  Aidha, Mheshimiwa Waziri aliagiza kikao cha dharura na Mtendaji Mkuu wa Bima pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Bima tarehe 16/8/2017 saa mbili na nusu asubuhi katika ofisi za BAKITA. Alisisitiza kuwa wahusika wanatakiwa kuhudhuria kikao hicho muhimu bila kukosa.
  Kaimu Ofisa Mawasiliano na Umma
  BAKITA