Habari na Matukio
BAKITA LATAKIWA KUIBUA VYANZO VIPYA VYA MAPATO NA KUSIMAMIA MATUMIZI YA KISWAHILI FASAHA.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa ametembelea Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na kuiagiza menejimenti ya Baraza kuibua vyanzo vipya vya mapato ikiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vya Kiswahili jijini Dodoma na Arusha, kuanzisha kozi fupi kwa Waandishi wa habari, makatibu muhtasi na Watanzania kwa ujumla.
Ameyasema hayo leo akiwa BAKITA ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
“Hii ni ziara ya kutembelea taasisi ambazo ziko chini ya wizara ninayoiongoza ili nijue maendeleo yake na kubadilishana mawazo na viongozi wa taasisi hii”, amesema Msigwa.
Amelitaka BAKITA kuongeza jitihada za kutangaza lugha ya Kiswahili kwani ndilo jukumu lake la msingi.
“Tutabidhaisha Kiswahili na tutasimamia Kiswahili fasaha kwa kuwa tunayo fursa ya kupeleka Kiswahili katika nchi zote duniani”, ameongeza Msigwa.
Aidha, amewataka Waandishi wa habari na Watangazaji kuona fahari ya kuzungumza Kiswahili fasaha.
“Kati ya mambo yasiyofaa ni kuona vyombo vya habari vinaharibu lugha ya Kiswahili, tushirikiane na wizara na BAKITA kutumia Kiswahili fasaha kwani sisi ndio wa kushika bendera yetu na kuipeperusha lugha fasaha ya Kiswahili”, amesema Msigwa.