Habari na Matukio

BAKITA LATEMBELEWA NA MABALOZI

Published

on

Baadhi ya Mabalozi walioteuliwa hivi karibuni na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, wamelitembelea Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ili kupitishwa katika Mkakati wa Taifa wa Kubidhaisha Kiswahili ndani na nje ya nchi.

Akiongea mbele ya mabalozi hao Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Bi. Consolata Mushi amesema kuwa lengo la mkakati huo wa miaka kumi (2022-2032) ni kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa ya mawasiliano mapana barani Afrika ili iweze kutumika kuleta maendeleo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ndani na nje ya Tanzania.

“Tunawaomba huko mnapokwenda muendeleze jitihada zinazofanywa na Serikali za kubidhaisha Kiswahili kwa kufungua vituo vya kufundisha Kiswahili kwa wageni. Ninyi ni watu muhimu katika kuitangaza lugha ya Kiswahili kimataifa hasa ikizingatiwa kwamba kwa sasa Kiswahili kimeendelea kuwa na watumiaji wengi zaidi duniani”, amesema Bi. Consolata.

Kwa upande wake kiongozi wa msafara huo Mhe. Balozi Khamis Omar amesema kuwa Kiswahili ni tunu ya Taifa la Tanzania na Serikali imesisitiza sana kwa balozi za Tanzania nje ya nchi kufanya jitihada maalumu za kukuza lugha ya Kiswahili na kuifanya kuwa bidhaa yenye tija kwa Taifa.

“Tunapongeza jitihada za taasisi na mashirika mbalimbali kwa kubadili sheria ya matumizi ya lugha ambayo ilikuwa inawapa watendaji uhuru wa kuchagua ama kutumia lugha ya Kuswahili au lugha ya kigeni katika kutoa maelezo ya bidhaa na shughuli zake badala yake sheria inaelekeza kutumia lugha ya Kiswahili na ya kigeni”, amesema Balozi Omar.

Aidha, ameahidi kwamba balozi hizo zitaendelea kuanzisha na kuimarisha vituo vya kufundisha Kiswahili kwa wageni ili kuendelea kukibidhaisha nje ya nchi.

Mabalozi waliofika BAKITA ni Mhe. Balozi Khamis Omar, Mhe. Balozi Dkt. Mohamed Abdalla, Mhe. Balozi Habibu Mohamed, Mhe. Balozi Hassani Mwamwetu, Mhe. Balozi Gelasius Byakanwa, Mhe. Balozi Meja Jenerali Ramson Mwaisaka, Mhe. Balozi Dkt. Bernard Kibesse na Mhe. Balozi Meja Jenerali Paul Simuli.

Mabalozi hao wanategemea kwenda katika nchi walizopangiwa hivi karibuni.

Trending

Exit mobile version