Habari na Matukio
“NIMERIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA BAKITA”- DKT. NDUMBARO
“NIMERIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA BAKITA”- DKT. NDUMBARO
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Damas Ndumbaro amesema kuwa ameridhishwa na juhudi zinazofanywa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi pamoja na kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kubidhaisha Kiswahili.
Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo leo tarehe 16, Oktoba, 2023 wakati wa ziara yake katika ofisi za BAKITA ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongoza wizara hiyo.
Amebainisha kuwa ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha kwamba lugha ya Kiswahili inatumika Umoja wa Mataifa kwa sababu mpaka sasa hakuna lugha yenye asili ya Afrika inayotumika katika Umoja huo.
“Nia ya Serikali ni kuhakikisha Kiswahili kinakuwa lugha ya tano duniani na kinaweza kutumika katika Umoja wa Mataifa. Tutaendelea kueneza Kiswahili duniani kwa kutumia balozi zetu zilizopo nje ya nchi, kuwa na vyuo vikuu vinavyofundisha Kiswahili na kutumia Diaspora wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi”, amesema Dkt. Ndumbaro.
Ameongeza kwamba dira ya ilani ya CCM inaelekeza kutoa ajira kwa vijana kupitia Kiswahili kwa sababu lugha ya Kiswahili kwa sasa ina fursa kubwa.
“Kiswahili kinavyoendelea kukua ndivyo ambavyo fursa zinavyoendelea kuambatana nacho ikiwa ni pamoja na kutangazwa duniani kote”, amebainisha Dkt. Ndumbaro.
Katika hatua nyingine Dkt. Ndumbaro amesema kuwa Serikali itafanya ushawishi katika mashindano ya soka Afrika yatakayofanyika mwaka 2027 katika nchi tatu za Afrika Mashariki ili yatangazwe kwa lugha ya Kiswahili.
“Tunataka Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) litumie Kiswahili katika mashindano hayo ili Watanzania na watu wote wafurahie fursa za Kiswahili”, ameongeza Waziri.
Awali, Katibu Mtendaji wa BAKITA, Bi. Consolata Mushi alimpitisha Waziri katika utekelezaji kazi wa Baraza ukiwepo Mkakati wa Taifa wa kubidhaisha Kiswahili ndani na nje ya nchi wa miaka 10 (2022-2032) ambapo alisema kuwa lengo la mkakati huo ni kuhakikisha kuwa Kiswahili kinafanywa kuwa bidhaa kitaifa, kikanda na kimataifa.
“Ubidhaishaji Kiswahili unakusudia kuifanya lugha hii iwe na tija kubwa kwa taifa, wataalamu na wazawa”, amesema Bi. Consolata.