English Post
“UCHUMI WA KIDIJITI MWAROBAINI WA AJIRA”- PROF. LUOGA
Na. Adabeth Mwanambuu-BAKITA
Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam wametakiwa kuendana na mabadiliko ya dunia katika mifumo ya teknolojia ili kujiongezea kipato na kujiajiri.
Hayo yamesemwa na Profesa Florens Luoga jijini Dar es Salaam katika kusanyiko la maandalizi ya mahafali ya wahitimu wa chuo hicho kwa mwaka 2022/2023.
“Kutokana na mabadiliko ya dunia kwa sasa Watanzania tunapaswa kujikita katika teknolojia ya kidigiti ili kuendana na uchumi wa kidijiti”, amesema Prof. Luoga
Amebainisha kuwa biashara kubwa na ya nafuu kwa sasa inafanyika kwa njia ya mtandao, njia inamfanya mwanadamu kupata bidhaa mahali alipo na kwa bei nafuu kuliko kuifuata kwa wazalishaji au wauzaji.
Amefafanua kuwa bidhaa za Kiswahili pia zinaingia katika mfumo wa mauzo ambayo yanaweza kuwasaidia wazalishaji wa bidhaa za Kiswahili kurahisisha bidhaa zao na kupata wateja wengi.
Bidhaa kama vitabu, ufundishaji wa Kiswahili mtandaoni, tafsiri na ukalimani na mambo mengine yahusuyo lugha ya Kiswahili yanaweza kuwafikia watumiaji wa kugha hiyo kwa njia nyepesi kabisa ambayo ni matumizi ya simu.
Prof. Luoga ameeleza kuwa vifaa vya kiteknolojia vimerahisisha mawasiliano ya kijamii na ya kiuchumi kwani ikiwa mtu hawezi kuendana na mabadiliko hayo hawezi kufanya biashara. Simu zimekuwa ndio kila kitu katika uchumi wa kidijiti kwa sasa.
“Watu wanaagiza, wananua na kuuza bidhaa kwa njia ya mtandao. Watu wanasoma maandiko mbalimbali kwa njia ya simu zao, ukibaki unategemea mtu aje kununua kitabu au gazeti au andiko lako utashindwa kufanya biashara. Jambo la muhimu ni kubadilika na kuendana na mahitaji ya kiulimwengu. Uza, nunua na agiza bidhaa mtandaoni.” Ameongeza Prof. Luoga.
Ameongeza kusema kuwa maendeleo hayo ya kiteknolojia yamesaidia kwa kiasi kikubwa katika ukusanyaji wa mapato kwa uhakika. Serikali na watu binafsi wanaweza kupata mapato kutokana na bidhaa zao pasi na kukumbana na changamoto ya upotevu au wizi wa fedha.
Akizungumzia changamoto za uchumi wa kidijiti, Prof. Luoga ameeleza kuwa uchumi huo usipochukuliwa kwa uangalifu unaweza kuleta utengano baina wa watu wenye uwezo wa kumiliki vifaa vya kiteknolojia na wale wasio na uwezo huo.
Naye Florian Kaijage, mwandishi na mtangazaji wa habari BBC, akishadadia suala la uchumi wa kidiji, amesema kuwa “mtaji mkubwa katika uchumi ni watu. Utakutana na watu, jitahidi kuwafanya watu wawe karibu yako. Lugha ndio kitu pekee kinachoweza kukufanya ukawa na mtaji wa watu. Ukiwa na watu utafanya mambo yako ya kidijiti kwa urahisi.”
Amebainisha kuwa soko lina mahitaji mengi na lina ushindani mkubwa, hivyo inabidi mtu afahamu anachotaka kufanya ili akifanye kwa ufanisi mkubwa na kuwa na nidhamu ya muda katika kitu hicho anachokifanya.
“Lugha ni muhimu sana katika kuwasilisha maudhui yako. Mathalani Kiswahili, kwa sasa kinahitajika sana duniani. Vyombo vingi vya habari vinahitaji wataalamu wa Kiswahili, hivyo ikiwa unahitaji kuwa bora katika ushindani wa soko la ajira, jifunze Kiswahili ukifahamu kwa kina ili uwe wa kipekee”, ameongeza Kaijage.
Chuo Kikuu cha Tumaini, kimeanzisha kozi ya Kiswahili kwa wanahabari ambayo imelenga kuwaandaa katika kuitumia lugha ya Kiswahili kwa ufanisi mkubwa.