Kuhusu BAKITA
Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ni Shirika la Umma ambalo kwa kawaida huwa chini ya Wizara yenye dhamana ya Utamaduni. Baraza liliundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 27 ya mwaka 1967 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 1983 na 2016. Sheria hii inalipa Baraza mamlaka ya kusimamia na kuratibu shughuli za wadau wote wanaokuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baraza liliundwa kutokana na mapendekezo makuu ya Kamati iliyoundwa kwenye kikao cha wataalamu wa lugha kilichoitishwa na Waziri wa Elimu Disemba 1961. Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuinua Kiswahili kama lugha ya Taifa. Baraza lilianza kazi na watumishi wanne katika ofisi za Wizara ya Elimu. Miongoni mwa kazi ya kwanza ya Baraza ilipendekezwa iwe kufasiri msamiati na misemo ya Sheria. Baadaye mwaka 1972, Baraza lilipata ofisi zake katika jengo la Shirika la Nyumba la Taifa, mtaa wa Samora na Azikiwe jijini Dar es Salaam, na mwaka 2012 Baraza lilihamia Kitalu Na.45 B, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.